Hebu vuta picha: Uko kwenye soko lenye hekaheka nyingi—labda ni Kariakoo (Dar es Salaam) au Gikomba (Nairobi). Unapita mbele ya duka, huna hata mpango wa kununua kitu chochote.
Ghafla, mfanyabiashara anakutazama, anatabasamu na kukuambia, "Kaka/Dada, hii rangi inaendana na wewe, hebu jaribu tu, hata usiponunua haina shida!" Dakika kumi baadaye, unajikuta unatoa pesa mfukoni na kununua vazi ambalo hukupanga kulinunua.
Je, unajua ni nini kimetokea hapo? Hujapigwa "tunguli" nawala sio kiini macho. Umetekwa na nguvu ya kitu kimoja kikubwa sana ambacho ni: Saikolojia.
Watu wengi wanadhani saikolojia ni jambo la wasomi tu wenye miwani kubwa maofisini au vyuoni, au ni sayansi inayowahusu watu wenye matatizo ya akili pekee. Lakini ukweli ni kwamba, saikolojia ni kama hewa unayovuta kila siku. Inatawala maisha yako ya kila siku kuanzia maamuzi yako, hisia zako, biashara na jinsi unavyoishi na watu.
1 Saikolojia ni Nini Hasa?
Kwa lugha nyepesi, Saikolojia (Elimunafsia) ni sayansi inayochunguza akili ya binadamu pamoja na tabia zake. Ni mbinu ya kuelewa kwanini watu wanafanya yale wanayoyafanya.
Kwanini unakasirika ukiwa na njaa? Kwanini ukisikia mlio wa ujumbe (notification) kwenye simu yako mwili unasisimka kutaka kujua ni nani amekutumia meseji? Kwanini ni rahisi kuahirisha kazi ngumu na kuamua kuangalia video za vichekesho mtandaoni?
Hayo yote ni maswali ambayo saikolojia inayajibu. Haimaanishi kuwa una tatizo; lakini inamaanisha kuwa wewe ni binadamu!
2 Jinsi Inavyogusa Maisha Yako Ya Kila Siku (Bila Wewe Kujua)
Waafrika, tuna utamaduni wetu wa kipekee, lakini kanuni za kisaikolojia zinatutawala wote, haijalishi wewe ni nani, kabila gani na unaongea lugha gani. Hapa kuna maeneo ambayo saikolojia inagusa moja kwa moja maisha yako kila uchao:
1. Kwenye Pesa na Biashara (Ushawishi)
Wafanyabiashara wajanja wanatumia saikolojia kila siku kuendesha biashara zao. Wanatumia Bei za Kuidanganya Akili: Umewahi kujiuliza kwanini bidhaa nyingi huuzwa Tsh 9,900 au Ksh 999 badala ya 10,000 kamili? Kisaikolojia akili yako inasoma namba ya kwanza, na inajidanganya kuwa "Ah, hii ni elfu 9," badala ya kuona elfu kumi. Kanuni ya Uhaba: Ukienda kununua kiwanja, nyumba au kupangisha chumba dalali atakuambia "Kuna mtu mwingine anakuja kutoa hela jioni hii, ukikikosa shauri yako.". Hofu ya kukosa fursa inakufanya ufanye maamuzi ya haraka.
2. Kwenye Mahusiano na Ndoa
Tunasema "Mapenzi ni hisia," lakini uhalisia ni kwamba mapenzi ni mchezo wa kisaikolojia. Zaidi ya asilimia 70 ya mawasiliano yetu hayahitaji maneno. Namna mwenza wako anavyokunja uso, anavyoepuka kukuangalia machoni, au anavyokaa mbali na wewe anapokuwa amekasirika; hiyo yote ni saikolojia ya mawasiliano, inaongea hata wakati ambao mweza wako hasemi chochote (Body Language).
3. Malezi na Makuzi ya Watoto
Waafrika tumelelewa kwenye mfumo wa matumizi makubwa ya kiboko. Lakini saikolojia inatufundisha jambo moja kubwa zaidi. Ukimsifia mtoto anapofanya vizuri (Positive Reinforcement), anapata hamasa ya kurudia hilo jambo zuri zaidi kuliko unapompiga anapokosea. Vipigo vya mara kwa mara hujenga hofu kwa wototo, na siyo heshima, na mtoto atajifunza kudanganya ili kukwepa maumivu ya vipigo, na ndio maana tunalea kizazi cha watoto waongo sana.
4. Afya ya Akili na Msongo wa Mawazo (Stress)
Maisha yana changamoto. Foleni za magari barabarani, ugumu wa uchumi, na presha za ndugu na wale wanao tutegemea. Ushawahi kujiuliza kwanini tunakuwa wepesi sana kutengeneza "Memes" na utani au vichekesho mtandaoni hata kukiwa na jambo zito la kitaifa? Kisaikolojia, hii inaitwa Coping Mechanism. Tunatumia ucheshi kupunguza maumivu ya kisaikolojia na kuifanya akili ipumue.
Nini cha Kufanya Sasa? (Ushauri wa Kitaalamu)
Kwa kuwa sasa unajua saikolojia siyo "uchizi" bali ni maisha yako ya kila siku, anza kuitumia kwa faida yako:
1. Jifunze Kusikiliza Kabla ya Kukurupuka Kujibu: Unapobishana na bosi wako au mwenza wako, vuta pumzi. Jiulize, "Kisaikolojia, nini kinamsumbua huyu mtu kwa sasa?"
2. Linda Afya Yako ya Akili: Kama unavyolinda simu yako isidondoke na kupasuka kioo, linda akili yako. Epuka kuruhusu taarifa hasi na watu wenye sumu kutawala hisia zako.
3. Tumia Ushawishi Chanya wenye manufaa: Unapotaka jambo lako lifanikiwe, usitumie nguvu. Tafuta kujua mtu unayehusiana naye anahofia nini, kisha zungumza naye kuanzia kwenye hiyo nukta.
3 Masomo Muhimu Katika Makala Hii
- Saikolojia ni hewa unayovuta kila siku; inatawala maamuzi, hisia, na jinsi unavyoingiliana na watu.
- Wafanyabiashara wanatumia mbinu za kisaikolojia (kama bei na uhaba) kushawishi maamuzi yako ya manunuzi.
- Mawasiliano katika mahusiano yanategemea sana lugha ya mwili (Body Language), sio tu maneno unayozungumza.
- Kusifia tabia nzuri kunajenga tabia bora kwa watoto kuliko kutumia adhabu pekee.
- Kuelewa akili yako mwenyewe inakupa uwezo wa kuyatawala maisha yako na kuyabadilisha kuwa mchezo ambao unajua jinsi ya kuushinda.